Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
WAZIRI NANAUKA AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO YENYE TH...

WAZIRI NANAUKA AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 371 TANGANYIKA, AHIMIZA VIJANA NA WANANCHI KUNUFAIKA NA FURSA ZA SERIKALI.

22 Jul, 2026
WAZIRI NANAUKA AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 371 TANGANYIKA, AHIMIZA VIJANA NA WANANCHI KUNUFAIKA NA FURSA ZA SERIKALI.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Dkt. Joel Arthur Nanauka, ameendelea na ziara ya kikazi mkoani Katavi ambapo leo ametembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya manendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, ikiwemo ujenzi wa bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Kabungu lenye thamani ya milioni 163.6 na ujenzi wa Zahanati ya Kitongoji cha Manyonyi kwa thamani ya milioni 190.

Mhe. Nanauka amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanganyika  kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili ianze kutoa huduma za malazi kwa wanafunzi sambamba na kuondoa changamoto ya wananchi kufuata matibabu umbali mrefu.

“Serikali imetenga pesa nyingi za kutekeleza miradi hii kutokana na umuhimu wake, hivyo basi ni muhimu ikamilike kwa wakati ili ianze kutoa huduma zinazokusudiwa” amesema Waziri Nanauka.

Katika hatua nyingine, Waziri Nanauka amewataka vijana kuchangamkia fursa za uwezeshaji zinazotolewa na serikali ikiwemo mikopo nafuu na tenda mbalimbali. Amesema hayo baada ya kutembelea kikundi cha vijana cha JOSA International Supply kuona kinavyoendesha shughuli zake baada ya kunufaika na mkopo wa asilimia 10 wa Halmashauri wenye thamani ya shilingi milioni 18.2 kikundi hicho kinajishughulisha na usambazaji wa umeme kupitia zabuni za TANESCO na biashara ya vifaa vya umeme.

Wananchi wameeleza kufurahishwa na uwekezaji wa serikali katika huduma za kijamii husani afya, Salehe Hamisi amesema kuwa kukamilika kwa zahanati ya Kitongoji cha Manyonyi kutawapunguzia wakazi wa kitongoji hicho umbali wa kufuata huduma za afya, huku Mariamu Yusufu akisema kuwa huduma za akina mama na watoto zitaimarika.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu amemhakikishia Waziri Nanauka kuwa ataendelea kushirikiana na uongozi wa Halmashauri katika kusimamia matumizi sahihi ya pesa za miradi inayoletwa na serikali wilayani humo, ili kutekeleza miradi ya huduma za kijamii kwa wananchi.