Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
VIJANA LINDENI AMANI, NDIO CHANZO CHA MAENDELEO YA...

VIJANA LINDENI AMANI, NDIO CHANZO CHA MAENDELEO YA TAIFA.

25 Jul, 2026
VIJANA LINDENI AMANI, NDIO CHANZO CHA MAENDELEO YA TAIFA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amewataka vijana nchini kuendelea kuwa walinzi wa amani na utulivu, akisisitiza kuwa mazingira ya amani ndio msingi unaowezesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo na ustawi wa Taifa.

Akizungumzawakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la Shule ya Msingi Kamwelwe katika Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi, Mhe. Nanauka amesema vijana wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika shughuli za uzalishaji na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na kuhatarisha usalama wa nchi.

"Serikali imeendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia programu mbalimbali. Nawasihi mtumie fursa hizo kujiajiri, kuongeza kipato na kutimiza malengo yenu, huku mkidumisha amani ambayo ndio msingi wa maendeleo ya Taifa," amesema Mhe. Nanauka.

Aidha, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo pamoja na uwezeshaji wa vijana ili kuongeza ustawi wa wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Katavi, Mhe. Thomas Kampala, amemhakikishia Waziri Nanauka kuwa jimbo hilo liko salama na lenye mshikamano, huku vijana wakishiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji zinazochangia ukuaji wa uchumi. Pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuuelekezea Mkoa wa Katavi fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoboresha maisha ya wananchi.