Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
NANAUKA AHIMIZA WANANCHI KUFUATA NGAZI ZA UONGOZI...

NANAUKA AHIMIZA WANANCHI KUFUATA NGAZI ZA UONGOZI KUTATUA KERO

25 Jul, 2026
NANAUKA AHIMIZA WANANCHI KUFUATA NGAZI ZA UONGOZI KUTATUA KERO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amewataka wananchi kutumia Serikali za Mitaa kama ngazi ya kwanza ya kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo migogoro ya ardhi, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kiutawala.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ipwaga, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Mhe. Nanauka amesema Serikali imeanzisha Serikali za Mitaa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha changamoto nyingi zinapatiwa ufumbuzi katika maeneo yao bila kulazimika kufuata viongozi wa ngazi za juu.

"Wananchi wanapaswa kuamini na kutumia mifumo ya Serikali iliyoanzishwa kwa ajili yao. Anzieni katika Serikali ya Kijiji na kata, kwani ngazi hizi zina mamlaka ya kushughulikia changamoto nyingi kabla ya kufikishwa katika mamlaka za juu," amesema Mhe. Nanauka.

Ameongeza kuwa kufuata utaratibu huo kutarahisisha utatuzi wa migogoro, kupunguza msongamano wa malalamiko katika ngazi za juu na kuongeza uwajibikaji wa viongozi wa maeneo husika.

Naye Mbunge wa Jimbo la Katavi, Mhe. Thomas Kampala, amesema kuwa anaendelea kushirikiana na viongozi wa Mkoa na Wilaya kuwapa wananchi elimu kuhusu taratibu za Serikali katika utoaji wa huduma za kiutawala. Amesema mikutano ya hadhara imekuwa jukwaa muhimu la kusikiliza kero za wananchi, kuzitafutia ufumbuzi na kuwajengea uelewa wa kufuata ngazi sahihi za uongozi.

Katika mkutano huo, Waziri Nanauka amepokea na kutatua changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi, zikiwemo migogoro ya ardhi, masuala ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na uboreshaji wa huduma za kijamii, huku akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati.