Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
VIJANA WAPEWA MWELEKEO MPYA; SERIKALI NA ASASI ZA...

VIJANA WAPEWA MWELEKEO MPYA; SERIKALI NA ASASI ZA KIRAIA ZASHIRIKIANA KUSUKUMA AJENDA YA MAENDELEO ENDELEVU.

28 Apr, 2026
VIJANA WAPEWA MWELEKEO MPYA; SERIKALI NA ASASI ZA KIRAIA ZASHIRIKIANA KUSUKUMA AJENDA YA MAENDELEO ENDELEVU.

Serikali kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia imeweka mkazo mpya katika kuwawezesha Vijana kiuchumi,Kijamii na kiteknolojia,huku changamoto za ajira na mitaji zikitajwa kuwa kikwazo kikubwa kinachohitaji hatua za haraka .

Hayo yamebainishwa katika Kongamano la pamoja lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano  wa Kimataifa wa Mwalimu Juliusi Nyerere Aprili27’ 2026 Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili hatma ya Maendeleo ya Vijana nchini.

Akifungua  na Kufunga Kongamano hilo Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais -Maendeleo ya Vijana, Mhe Athur Nanauka amesisitiza dhamira ya Serikali katika kuhakikisha vijana wanakuwa Kitovu cha Maendeleo kupitia  Sera,mipango na Ushirikiano mpana wa Wadau.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea  kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana, huku ikiimarisha mshikamano,maadili, na matumizi ya Teknolojia kwa vijana.

Pamoja na mafanikio yaliyopo,Waziri Nanauka amebainisha changamoto zinazoendelea kuwakabili Vijana,zikiwemo ukosefu wa ajira,ufinyu wa mitaji na pengo la ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Hata hivyo ameeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo utoaji wa mikopo kwa Vijana, elimu ya ujasiliamali,pamoja na juhudi za kuboresha mifumo ya kuwawezesha vijana kiuchumi ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine.

Kwa upande wao wadau, wameeleza  sera zilizopo zinawafikia vijana wote hasa walioko katika makundi maalum,huku vijana wakihimizwa kutumia kikamilifu fursa zilizopo.

Aidha ushirikishwaji wa vijana katika maamuzi yanayowahusu uliwekwa kama kipaumbele muhimu katika kufanikisha Maendeleo Jumuishi na endelevu.

Kongamano hilo lilijumuisha uwasilishaji wa mada mbalimbali ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana(Toleo la 2024,nafasi ya Asasi za Kiraia,pamoja na majukumu ya Taasisi kama, Baraza la Taifa la Vijana na Ofisi ya Msajili wa NGOs.Majadiliano ya wazi  yaliwapa washiriki nafasi ya kubadilishana uzoefu na kutoa mapendekezo yenye lengo la kuboresha vijana nchini.

Akihitimisha Kongamano hilo,Waziri Nanauka  amesisitiza umuhimu wa usajili rasmi wa mashairika/na Asasi za kiraia ,Mawasiliano sahihi na matumizi ya lugha rafiki kwa vijana ili kuwafikia kwa ufanisi zaidi.

Amewahamasisha Vijana kuchangamkia fursa zilizopo kama mikopo ya riba nafuu huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya utafiti kuona uwezekano wa kuanzisha Benki ya Vijana.

Pamoja na hayo amehimiza vijana kuwa na uthubutu, kujiamini na kuchukua hatua katika kujenga maustakabali wao.Kongamano hilo limekuwa chachu ya kuongeza juhudi katika kuwajengea vijana uwezo,kuwaunganisha na fursa sahihi na kuimarisha usirikiano na serikali pamoja na wadau wengine.Msukumo uliotolewa unaashiria mwanzo mpya wa safari ya maendeleo ya vijana  yenye mwelekeo thabiti na matokeo chanya.