Serikali inaendelea kuratibu mipango ya kuwawezesha vijana kunufaika na fursa za kiuchumi kupitia sekta ya utalii na ujasiriamali, kwa lengo la kukuza ajira, kujiajiri na ushiriki wao katika maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea vikundi vya ujasiriamali vya vijana katika Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kupitia kaulimbiu ya “Punguza Itifaki, Tukutane Site.” Amesema Ofisi yake inaratibu ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuandaa programu maalumu zitakazowawezesha vijana kutumia vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yao kujipatia kipato na kukuza biashara zao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Enock Koola, amewashukuru vijana kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo, ikiwemo kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya utalii. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya vijana na Serikali katika juhudi za kuboresha sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika uchumi wa vijana.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Ndugu Shadrack Mohamed Mhagama, amesema Halmashauri ina utaratibu wa kuwajengea vijana uwezo wa kuandaa maandiko ya miradi. Amewataka kuzingatia masharti na kuwasilisha miradi yenye tija ili kunufaika na mikopo ya asilimia 15 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Kwa upande wa vijana, Vicent Bajuta ameiomba Serikali kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha kujiajiri kupitia sekta za utalii na michezo. Naye Baraka Richard Marenge amewahimiza vijana kushiriki katika vikao vya maendeleo ili kuwasilisha changamoto zao na kutoa mawazo kuhusu maendeleo ya maeneo yao.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana na vijana kupitia vikundi vyao, kwa kusikiliza mahitaji yao, kubaini changamoto na kuratibu hatua za kuwaunganisha na fursa za kiuchumi zinazoweza kukuza ujasiriamali na kujiajiri.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nana...
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nana...
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeitaka Ofisi ya Rais...
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imepongeza maandalizi...
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba...