Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
WAZIRI MKUU AWATAKA VIJANA KUTUMIA BUNIFU KUTATUA...

WAZIRI MKUU AWATAKA VIJANA KUTUMIA BUNIFU KUTATUA CHANGAMOTO ZA TAIFA

13 Oct, 2026
WAZIRI MKUU AWATAKA VIJANA KUTUMIA BUNIFU KUTATUA CHANGAMOTO ZA TAIFA

WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka vijana kutumia bunifu zao kutatua changamoto zinazolikabili taifa, hususan katika utunzaji wa mazingira na kilimo, ili kuchochea maendeleo na kuongeza fursa za kiuchumi nchini.

Mhe. Nchemba ameyasema hayo alipotembelea banda la vijana wabunifu katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika Viwanja vya Ndua, Sumbawanga, mkoani Rukwa, kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026. Amesema bunifu hizo zimeonesha uwezo wa vijana kujiajiri, kuajiri wengine na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Katika ziara hiyo, Mhe. Nchemba ametembelea vikundi nane vya vijana vinavyozalisha bidhaa katika sekta mbalimbali, zikiwemo kilimo, afya na teknolojia, ambavyo kwa pamoja vimeajiri vijana zaidi ya 900, hatua inayoonesha mchango wa ubunifu katika kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.

Miongoni mwa vikundi alivyotembelea ni Shule Yetu.com cha Dar es Salaam, kilichobuni saa maalumu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watoto na kurahisisha uokozi wao wanapokabiliwa na hatari; Trash to Treasure cha Rukwa, kinachotengeneza vifaa vya kufundishia kwa kurejeleza taka; Iphytos cha Arusha, kinachozalisha dawa za binadamu; CutOff Recycle, kinachotumia nywele za binadamu kutengeneza mbolea; na Ukwavila Group, kinachojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya chakula.

Aidha, Waziri Mkuu amempongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, kwa juhudi za kuweka mipango ya kuwawezesha vijana kupitia ubunifu na shughuli za uzalishaji. Maonesho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana,” yakilenga kuonesha uwezo wa vijana na fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta mbalimbali.