Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
KAMATI YA BUNGE: YES IWE CHANZO CHA TAARIFA ZA VIJ...

KAMATI YA BUNGE: YES IWE CHANZO CHA TAARIFA ZA VIJANA

20 Oct, 2026
KAMATI YA BUNGE: YES IWE CHANZO CHA TAARIFA ZA VIJANA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeitaka Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kuwa Mfumo wa Youth Empowerment System (YES) unakuwa chanzo cha kuaminika cha taarifa zinazohusu vijana nchini, zikiwemo fursa za ajira, mafunzo na programu za uwezeshaji.

Maelekezo hayo yametolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Rejina Christopher Malima (Mb), Oktoba 20, 2026, jijini Dodoma, wakati Kamati ikipokea taarifa ya utekelezaji wa Mfumo huo kutoka Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana. Taarifa hiyo imeeleza kuhusu usanifu, utengenezaji na uendeshaji wa mfumo huo, pamoja na namna utakavyosaidia kuratibu fursa na programu za maendeleo ya vijana nchini.

Mhe. Malima ameipongeza Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa kutumia teknolojia kuwafikia vijana, akieleza kuwa hatua hiyo utarahisisha upatikanaji wa taarifa, kupunguza gharama na kuongeza ufanisi wa huduma. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha Mfumo wa YES unakuwa na taarifa sahihi na zinazosasishwa mara kwa mara ili vijana wapate fursa zinazowahusu kwa wakati.

Akichangia katika kikao hicho, Mjumbe wa Kamati, Mhe. Kafiti William Kafiti, amesisitiza umuhimu wa kutumia Mfumo wa YES kuwaunganisha vijana na fursa za maendeleo. Amesema mfumo huo unapaswa kuwawezesha vijana kushiriki katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuwa wamiliki wa uchumi, huku wakitumia fursa zilizopo kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mhe. Paschal Lutandula, ameipongeza Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa hatua za kuboresha mifumo ya teknolojia, akisisitiza umuhimu wa Mfumo wa YES kusomana na mifumo mingine ya Serikali ili kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa, kuimarisha uratibu wa fursa na kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi kuhusu programu za maendeleo zinazowahusu.

Akijibu hoja za wajumbe katika kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha Mfumo huo ili kuongeza ufanisi katika uratibu wa fursa na programu za maendeleo ya vijana, ikiwemo kuanzisha huduma ya USSD itakayowawezesha vijana wasio na simu janja, hususan wanaoishi vijijini na maeneo ya mbali na miji, kupata taarifa na kunufaika na fursa za maendeleo ya vijana. Aidha, Mhe. Nanauka ameishukuru Kamati hiyo kwa maoni na ushauri iliyoutoa, akieleza kuwa utasaidia kuboresha mfumo huo na kuhakikisha kuwa unatekeleza malengo yake kwa ufanisi unaokusudiwa.