Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
NANAUKA ASISITIZA ELIMU YA FEDHA KWA VIJANA

NANAUKA ASISITIZA ELIMU YA FEDHA KWA VIJANA

26 Oct, 2026
NANAUKA ASISITIZA ELIMU YA FEDHA KWA VIJANA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amesisitiza umuhimu wa elimu ya fedha kwa vijana ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kutumia rasilimali zao kwa ufanisi na kuchangamkia fursa za uwekezaji kwa ajili ya kujenga ustawi wa kiuchumi.

Ameyasema hayo alipokuwa Mgeni Rasmi katika Fainali za Mashindano ya Uwekezaji kwa Wanafunzi ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE Scholar Investment Challenge) msimu wa 2025/2026, zilizoambatana na mahafali ya Kundi la Pili la wahitimu wa Cheti cha Uwekezaji na Biashara ya Dhamana (Certificate in Securities Investment and Trading – CerSIT).

Nanauka amesema uelewa wa masuala ya fedha huwasaidia vijana kutambua fursa zilizopo katika masoko ya mitaji na kupanga mipango ya muda mrefu. Ameipongeza DSE kwa kuendeleza programu hiyo, ambayo tangu mwaka 2014 imewafikia washiriki 50,000, huku msimu wa 2025/2026 ukishirikisha washiriki 7,883.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa na nidhamu, uvumilivu na mtazamo wa muda mrefu katika kufikia malengo yao ya kifedha, badala ya kutarajia mafanikio ya haraka. Ameeleza kuwa teknolojia, ikiwemo majukwaa ya kidijitali kama Hisa Kiganjani, inarahisisha upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji na kupanua fursa za vijana kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Katika hafla hiyo, Nanauka amewapongeza wahitimu wa CerSIT kwa kupata ujuzi katika masuala ya dhamana na masoko ya mitaji. Ameeleza kuwa kupanua elimu ya fedha na kuwajengea vijana uwezo wa kutumia fursa za kiuchumi ni sehemu ya juhudi zinazochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani unaochochewa na teknolojia na ubunifu.