Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
WAZIRI MKUU NCHEMBA ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA...

WAZIRI MKUU NCHEMBA ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA VIJANA VIWANJA VYA NDUA

13 Oct, 2026
WAZIRI MKUU NCHEMBA ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA VIJANA VIWANJA VYA NDUA

-Asifu bunifu za Vijana zinazozalisha ajira
-Atoa ahadi ya kuongeza bajeti ya Vijana Kila Mwaka
-Apongeza,aridhishwa na Maandalizi kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru,2026

Na Byarugaba Innocent-ORMV 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Mwigulu Lameck Nchemba amefika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa kuangalia maandalizi ya Kilele cha Mwenge wa Uhuru,2026 kinachotarajia kufika tamati tarehe 14 Oktoba,2026 kwenye Viwanja vya Nelson Mandela.

Akisoma taarifa ya maandalizi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe.Joel Arthur Nanauka amesema maandalizi yote yamekamilika kwa matukio mawili ikiwemo maandalizi ya Misa Maalumu ya kumwombea Baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere itakayofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Mt.Epifania Jimbo la Sumbawanga Kuanzia saa 12 asubuhi.

Wakati huo huo Mhe.Nchemba ametembelea Maonesho ya wiki ya Vijana yanayoendelea kwenye Viwanja vya Ndua yaliyoanza tarehe 8 Oktoba na kufunguliwa rasmi tarehe 10 Oktoba,2026 na Waziri wa Elimu Prof.Adolf Mkenda.

Akiwa kwenye banda la Vijana Wabunifu ameridhishwa na ubunifu kwa Vijana unaolenga kubadili mitazamo na fikra za Watanzania kuwa Vijana wanaweza kuendesha na kumiki Uchumi wa Tanzania.

Amempongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe.Joel Arthur Nanauka kwa kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kubadili Wizara ya Vijana kuwa ya Uzalishaji.

Aidha,Mhe.Nchemba ameeleza kuwa Serikali inakusudia kuhakikisha kuwa shughuli za Vijana zinapewa kipaumbele  na itaendelea kuongeza bajeti Kila Mwaka kwa ajili ya kuwawezesha Vijana.

Waziri Mkuu ametembea vikundi 8 vya Vijana Wabunifu ambavyo vimeajiri Vijana zaidi ya 900.

Vikundi hivyo ni Kikundi cha Kidot Comfort cha Dodoma chenye Vijana 5 kinachojishughulisha na uzalishaji na uuzaji wa bidhaa za urembo,Ukwavila Youth Group Vijana 150 cha Mbarali Mbeya kinacholima zao la Mpunga,Shule yetu.com Vijana 25 cha Dar es Salaam kilichobuni  saa ya uokozi na  Kikundi cha Trash to Treasure cha Arusha kinachotengeneza nyenzo za kufundishia kutokana na taka chenye Vijana 100.

Vikundi vingine ni CutOff Recycle chenye kauli mbiu ya "Tuletee nywele, tukulipe cha Arusha kinachotengeneza Mbolea hai za maji kutokana na malighafi za nywele chenye ajira 355,Iphytos wanaotengeneza Dawa za binadamu cha Arusha chenye ajira 30,Sotch tech Limited cha Arusha kinachotengeneza bidhaa za kikapu chenye ajira 210 na Kikundi cha Bize Group cha Sumbawanga  kinachojishughulisha na utengenezaji wa Batiki,Sabuni za maji na Karanga za Mayai.

Maadhimisho ya wiki ya Vijana,2026 yanachagizwa na Kaulimbiu isemayo "Mazingira tofauti,fursa sawa kwa Vijana"

Mhe.Dkt.Nchemba amewashuru Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Wizara ya Kazi,Ajira, Vijana na Uwezeshaji-Zanzibar na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa maandalizi mazuri kuelekea Kilele cha Mwenge wa Uhuru,2026